Ilikuwa ni kazi ambayo nilijua kabisa rafiki yangu Joyce angeweza
kuifanya, moja kwa moja nilimpigia simu na kumjulisha ili aweze kupeleka
vyeti vyake. Ni muda mrefu Joyce alikuwa akihangaika huku na kule
kutafuta ajira hivyo niliamua kumsaidia ili aweze kufanikiwa kupata
kazi. Baada ya kumueleza Joyce alifurahi sana na haraka alikwenda
kupeleka vyeti vyake na baadaye alifanyiwa usaili, na baada ya wiki
mbili tu alifanikiwa kupata kazi katika kampuni ya Sigara. Maisha
yaliendelea na sasa wote tulikuwa na kazi. Siku moja nikiwa nyumbani
nimepumzika Joyce alifika huku akionekana kuwa mwenye furaha sana "Mary
rafiki yangu, sasa mambo yangu ni mazuri, yaani hapa nilipo ninafuraha
sana, yaani hata sijui nianzie wapi kukueleza".
Nilimtizama huku
nikionyesha tabasamu zito nikiwa na shauku kubwa la kutaka kujua kwanini
Joyce alikuwa amefurahi kiasi kile "Ehee niambie rafiki kuna nini tena"
Aliguna kidogo kisha akasogea na kuketi karibu yangu huku akinionyesha
karatasi ambayo ilikuwa na maandishi ambayo nilishindwa kuyasoma kwa
haraka kwasababu Joyce alikuwa akihangaisha mikono yake bila kutulia,
"Yaani Mary mwenzio naenda Marekani umeona hii barua ni kwamba kuna
nafasi za kazi, zimetoka hivyo na mimi nimejaza fomu na hivyo
nimechaguliwa kwaajili ya kwenda kusoma na kufanya kazi, hapa nilipo
ninafuraha isiyo na kifani".
Nilifurahi sana kusikia rafiki yangu
kipenzi ndoto zake zinakamilika "Hongera sana (my dear)mpendwa, Mungu
akutangulie, katika kila jambo hiyo ni hatua kubwa sana, sasa mbona
hukuniambia na mimi mapema ningejaribu bahati yangu?" Joyce alicheka na
kusema "Unajua hizi nafasi zilikuwa chache na maalumu kwa wafanyakazi
wa kampuni ninayofanyia kazi hivyo hata ningekuambia usingeweza
kufanikiwa" Tulizungumza sana siku hiyo na nilimtakia kila la heri
baadaye aliondoka.
Baada ya wiki chache kupita Joyce akiwa
anajiandaa kusafiri, siku hiyo nilikutana na kaka mmoja anaitwa Roy
ambaye alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya sigara kaka huyu tulikuwa
tukifahamiana muda mrefu sana na ndiye aliyenisadia kumuunganishia
Joyce kupata ajira katika kampuni yao, tulisalimiana kisha akaanza
kusema "Mary, mbona umepuuzia bahati ya kwenda kusoma Marekani, kwanini
sasa ulikataa kujaza fomu na nilimpa Joyce akuletee.
Nilistaajabu
aliponiambia kuwa huna mpango wa kuendelea kusoma, na tena unataka
kuolewa hivi karibuni, kimya kimya rafiki yangu hata kunifahamisha"
Nilimsikiliza Roy kwa umakini maneno aliyokuwa anazungumza nikabaki
nimepigwa na butwaa na kunyamaza kimya kidogo kisha nikamjibu "Ati nini,
mimi kuolewa, wapi na nani? Halafu mbona Joyce hakuwahi kunieleza
chochote kuhusu, kujaza fomu ya kwenda kusoma nje ya nchi, na pia
nilimuuuliza siku aliyokuja kunipa taarifa kuwa anakwenda Marekani
kusoma, akaniambia nafasi hizo ni kwaajili ya wafanyakazi wa kampuni
yenu pekee, sasa nashangaa kuona wewe unaniambia mimi nimechezea bahati
inamaana Joyce ni mbinafsi kiasi hicho,
Ama kweli shukurani ya
punda mateke, na katika maisha tenda wema uende zako usingoje shukurani,
yaani hakumbuki wema niliomtendea, kumtafutia kazi hadi kafanikiwa
leo hii anashindwa kunishirikisha katika jambo kama hili haya bwana kama
ndivyo alivyoamua" Roy alinitizama kwa macho ya upole na kusema "Daah
pole sana, Mary, ila yote maisha, wewe achana naye endelea na maisha
yako kwani kuna leo na kesho, na katika maisha binadamu shida haziishi,
leo unaweza kumsaidia mtu akafikiri ndiyo amemaliza kila kitu
akakupotezea, na kukuona hauna msaada tena lakini ipo siku atarudi
kuomba msaada wako tena huku akijuta kwa alichokutendea."
Nilisikitika sana siku hiyo, nilitamani kumpigia simu kumueleza lakini
niliamua kukaa kimya kutokana na ushauri wa Roy, na kweli Mungu alivyo
wa ajabu safari yake haikufanikiwa kwani kuna vigezo alikuwa
hajakamilisha, na baada ya miezi mitatu, alikuja akasimamishwa kazi
kutokana na ukosefu wa nidhamu kazini, alinifuata na kunieleza, huku
akiniomba nimsaidie kutafuta kazi, siku hiyo sikutaka kubaki na dukuduku
nililokuwa nalo moyoni ilinibidi nimuweke wazi kwa kile alichonitendea
kipindi cha nyuma, alinisikiliza huku akiniomba msamaha, bila hiyana
nilimsamehe, lakini moyoni mwangu nilijua kabisa Joyce siyo rafiki mzuri
kwani nimbinafsi anataka kufanikiwa yeye pekee na si vinginevyo, na
akishafanikiwa hakumbuki alipotokea.Ubinafsi ni kitu kibaya sana kwani
katika maisha ni vyema kusaidiana katika kila jambo kwani huwezi kujua
kesho itakuwaje na nani atakayekusaidia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni