UNAJUA jina la mwanamume mwenye nguvu
kuliko wote? Ni mwamuzi Samsoni. Yehova anampa Samsoni nguvu hizo. Hata
kabla ya Samsoni kuzaliwa, Yehova anamwambia mama yake hivi: ‘Upesi
utazaa mwana. Ataongoza kuokoa Israeli kutokana na Wafilisti.’
Wafilisti ni watu wabaya wanaoishi Kanaani. Wana wanajeshi wengi, na
wanawaumiza Waisraeli sana. Wakati mmoja, Samsoni anapokwenda kwa
Wafilisti, simba mkubwa anatokea akinguruma kukutana naye. Lakini
Samsoni anamwua simba huyo kwa mikono yake tu. Pia anaua mamia ya
Wafilisti wabaya.
Baadaye Samsoni anapendana na mwanamke,
Delila. Viongozi Wafilisti wanaahidi kwamba kila mmoja wao atampa Delila
vipande 1,100 vya fedha akiwaambia kinachompa Samsoni nguvu nyingi
hivyo. Delila anataka fedha zote hizo. Yeye si rafiki wa kweli wa
Samsoni, wala wa watu wa Mungu. Anazidi kumwuliza Samsoni kinachompa
nguvu nyingi hivyo.
Mwishowe, Delila amshawishi Samsoni. Naye Samsoni anamwambia siri ya
nguvu zake, akisema: ‘Mimi sijanyolewa nywele. Tangu kuzaliwa kwangu,
Mungu alinichagua niwe mtumishi wake wa pekee, yaani, Mnadhiri.
Nikinyolewa nywele, nitapoteza nguvu.’
Delila anapojua hayo,
anamlaza Samsoni katika paja lake. Kisha amwita mtu aje amnyoe nywele.
Samsoni anapoamka, anakuta amepoteza nguvu. Ndipo Wafilisti wanakuja
kumkamata. Wanamwondoa macho yake mawili, na kumfanya mtumwa wao.
Siku moja Wafilisti wanafanya karamu kubwa ili waabudu Dagoni mungu
wao. Wanamtoa Samsoni gerezani ili wamcheke. Wakati huo, nywele za
Samsoni zimekua tena. Samsoni anamwambia kijana anayemwongoza kwa mkono:
‘Acha nishike nguzo za jengo hili.’ Kisha Samsoni anamwomba Yehova ampe
nguvu, naye anashika nguzo hizo. Anapaza sauti hivi: ‘Acha nife pamoja
na Wafilisti.’ Wafilisti wanaokula karamu ni 3,000. Samsoni anapoegemea
nguzo hizo, jengo laanguka na kuua watu wote hao wabaya. Waamuzi sura ya 13 mpaka 16.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni