
Nilikuwa katika wakati mgumu sana, kwani hakuna aliyekuwa akinijali, lakini sikukata tamaa kwakuwa niliamini Mungu yupo pamoja nami. Kuna wakati nilijikuta nakata tamaa kutokana na watu wengi kunizungumzia maneno yasiyokuwa na ukweli wowote. Maisha yangu yalikuwa yamezungukwa na marafiki wengi ambao kwa kiasi kikubwa nilikuwa nikiwaonyesha upendo na kuwaamini kuwa ni watu wa muhimu sana katika maisha yangu, Lakini kumbe haikuwa vile ninavyofikiria walikuwa wamejivika ngozi ya kondoo lakini mioyo yao ikiwa imejaa chuki juu yangu. |
Katika Maeneo ya Vijana Kinondoni
jijini Dar es salaam nilikuwa nikishi na Mama yangu mkubwa, kwani
sikubahatika kuishi na wazazi wangu Baba na Mama yangu walifariki nikiwa
mdogo sana. Mama yangu mkubwa alinilea vizuri sana hadi nilipomaliza
elimu yangu ya sekondari, na kufanikiwa kuanza chuo cha uhasibu. Nikiwa
chuoni nilikutana na marafiki mbalimbali.
Saida alikuwa ni rafiki yangu kipenzi
pale chuoni. Siku moja nikiwa najisomea Saida alikuja na kusema "Rozi
rafiki yangu, kuna jambo nataka kukuambia, lakini mwenzangu usije
ukamwambia mtu yeyote kuwa mimi ndiye niliyekueleza jambo hili"
Ilinibidi nishangae na kusema "Ni jambo gani hilo? Mbona unaniweka roho
juu. "Maneno yameenea hapa chuoni, watu wanakusema sana vibaya, yaani
sijui nianzie wapi kukueleza." Moyo wangu ulishtuka nikawa nimebaki
nashangaa "He! Watu wananisema vibaya? Kwani mimi nimefanya nini? Mbona
unanishangaza Saida embu kuwa muwazi uniambie ni kitu gani kinaendelea".
Saida aliguna kidogo nakusema "Rafiki
yangu, hivi ni kweli una uhusiano wa kimapenzi na mwalimu wa hesabu.
Mr Ngowi, ndiyo maana unafaulu vizuri somo lake?" Ilinibidi niweke
daftari langu pembeni na kusema "Eti nini Saida, kina nani wanasema
hivyo, jamani mbona watu wanapenda kuzungumza maneno ya uongo, mimi sina
uhusiano wowote na mwalimu Ngowi" Saida akacheka nakusema "Basi watu
wengi hapa chuo wanajua ni kweli na anayesambaza hayo maneno ni Lina,
ila chonde chonde usije kunitaja" Nilijisikia vibaya sana siku hiyo
kwani ukweli ni kwamba sikuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na
mwalimu.
Siku zilivyozidi kwenda maneno
yaliendelea na Saida alikuwa akija na kunieleza maneno ambayo
yanzungumzwa kuhusu mimi. Nilivumia hali hiyo bila yakumuuliza mtu
yeyote kwani nilikuwa sipendi ugomvi.Siku ya jumamosi na jumapili mara
nyingi nilikuwa nikienda kushinda nyumbani. Ilikuwa ni jumamosi moja
ambapo nilienda nyumbani na kumkuta mama yangu mkubwa akiwa amekasirika
sana. Nilimsalimia lakini hakuniitikia jambo ambalo niliona siyo la
kawaida.
Nilijaribu kumsalimia tena ndipo
aliponyanyuka na kunipiga kibao katika paji la uso wangu " Wewe
mwendawazimu, mimi nakulipia ada, halafu unaenda kufanya mambo ya ajabu
chuoni, hivi wewe ni mtu wa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwalimu
wako? Tena nimesikia huwa haulali chuoni kila siku unakuja kuchukuliwa
na wanaume tofauti, yaani unabadilisha wanaume kama nguo. Hivi hii tabia
ya ukahaba umeipata wapi?" Nilibaki nimeduwaa huku nikmisema "Hapana
Mama mimi sina tabia hiyo, siwezi kufanya hivyo, unanionea Mama" Nililia
kwa uchungu kwani Mama aliendelea kunigombeza huku akinipiga makofi ya
usoni bila ya kunisikiliza.
Maisha yangu yalikosa furaha kwani kila
kukicha yalikuwa yakiibuka mambo tofauti, lakini sikujua nani ambaye
anaweza kunifanyia yote haya. Kwani moyoni mwangu nilikuwa najua
sikuwahi kumkosea mtu yeyote.
Baada ya wiki mbili huku nikiwa sina
maelewano mazuri na familia yangu.Siku hiyo nilikuwa chumbani
nimepumzika pale chuoni alikuja Lina huku akiwa na kikosi cha marafiki
zake. "Tumechoshwa na maneno yako, Rozi wewe mwanamke ni mnafki sana,
kwanini unapenda kutufuatilia maisha yetu, unanisema vibaya kwa watu
kuwa mimi na uhusiano wa kimapenzi na walimu, eti ndiyo maana nafaulu
vizuri, ukaona haitoshi ukaenda kumwambia mpenzi wangu mimi namsaliti.
Kwanini unanifuatilia au unamtaka mpenzi wangu?". Aliongea Lina kwa
sauti ya jazba.
Nilinyanyuka pale kitandani na kuuliza
"Mbona siwaelewi, Eti unasema mimi nakusema vibaya, hivii unajua
unanishangaza wewe Lina yaani wewe unavyonizungumzia mimi vibaya,
unampelekea maneno ya uongo hadi Mama yangu mkubwa, umeona haitoshi
unataka kunisingizia mimi nakusema vibaya." Baada ya mimi kusema hivyo
wote walinyamaza kimya kwa muda huku wakitazamana, mmoja wao akauliza
"Nani amekuambia hayo maneno, acha uongo Lina hajawahi kukusema vibaya"
Kutokana na hasira nilizokuwa nazo kwa
wakati huo niliamua kumtaja Saida, ndipo wote wakabaki wakishangaa kumbe
Saida huyohuoyo ndiye aliyekuwa anawapelekea maneno kwamba mimi
namzungumzia vibaya Lina. Kwa wakati huo Saida alikuwa hayupo
tulimsubiri hadi aliporudi na sasa kila mmoja alimvamia kwa maneno
makali huku wakimwimbia kwa tabia yake mbaya ya kusema uongo na
kuchonganisha watu. Nilijisikia vibaya sana kwani mtu niliyemuamini kama
rafiki yangu ndiyo alikuwa na nia ya kunichonganisha na marafiki hadi
familia yangu. Aliniomba msamaha, mwanzoni ilikuwa ni vigumu kumsamehe
lakini baadaye niliamua kumsamehe na maisha yanaendelea SIJAPOTEZA
FURAHA YANGU.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni