"Asante sana shemeji Beni kwa msaada
ulionipa, lakini nilikuwa naomba uniongezee kiasi cha shilingi laki tano
tu, kuna jambo nataka kulifanya, nimepungukiwa kidogo, naimani
utanisaidia". Alikuwa ni shemeji yangu ambaye ni kwa kipindi kirefu
nimekuwa nikimsaidia kuendeleza biashara zake, kwa wakati huo nilikuwa
sina kiasi hicho cha fedha "Ningependa kukusaidia shemeji lakini hali
yangu kiuchumi kwa sasa imeyumba ila usiwe na shaka nitafanya mikakati
ndani ya siku mbili tatu nitakupa hiyo pesa.lakini shemeji kuwa makini
sana na utumiaji wa pesa kwani kwa sasa pesa imekuwa ngumu kupatikana
hivyo ni vyema ukawa makini sana katika biashara yako". Baada ya
kumaliza mazungumzo shemeji alinielewa na kuondoka.
Kesho yake asubuhi ilikuwa ni siku ya
jumamosi ambapo siku hiyo si kwenda kazini, alikuja dada yangu akiwa
pamoja na mtoto wake mdogo wa kike. "Habari za masiku dada, karibu
sana" Dada alinitizama huku akisema "Kaka habari yangu si njema kwani
hapa nilipo, nimekuja kwako nina shida mtoto amerudishwa nyumbani
kwasababu ya anadaiwa ada, sasa kaka naomba unisaidie shilingi laki tatu
niweze kumrudisha mjomba wako shule, yaani hapa nilipo sina mtu
mwingine wa kumtegemea zaidi yako".
Nilikuwa nimeketi pale sebuleni huku
nikiwaza na nafsi yangu "Mhhh hapa nilipo leo nimeamka nina shilingi
elfu kumi na tano tu mfukoni mwangu sasa nitawezaje kumsaidia dada
yangu" Nilimtizama dada na kusema "Daah, hali ni mbaya sana dada yangu,
umenikuta sina pesa kabisa lakini embu subiri naweza kumkopa rafiki
yangu kiasi hicho cha pesa ili mtoto aende shule." Nilimpigia simu
rafiki yangu anaitwa Zuberi na kumuomba anikopeshe pesa kidogo, kwa
bahati nzuri nilifanikiwa hivyo nilimpa kiasi kile cha fedha dada.
Baada ya dada yangu kuondoka mke wangu
alikuja akiwa ametoka sokoni "Mume wangu imekuwa ni vizuri nimekukuta
kwani mama amenipigia simu alikuwa anataka kuongea na wewe" Basi moja
kwa moja mke wangu akampigia simu Mama mkwe wangu kisha akanipa simu
niongee naye. "Shikamoo Mama habari za hapo nyumbani" Mama aliitika kwa
sauti ya unyonge "Habari si njema mwanangu mwili unaniuma sana, halafu
sina pesa kabisa, naomba unitumie hela ya kununua mchele na sukari
pamoja na ya kwenda Hospitali" Nilikuwa nikimsikiliza kwa umakini na
baadaye nilimuahidi kuwa nitamtumia pesa kwaajili ya matibabu na
chakula. Nilikuwa sina hela ilinibidi nikope pesa kwaajili ya kumtumia
mama mkwe.
Baada ya siku tatu kupita yule shemeji
yangu alinipigia simu na kunikumbusha kile kiasi cha pesa alichoniomba,
kwa bahati nzuri siku hiyo nilikuwa nimefanikiwa kupata pesa katika
biashara zangu hivyo sikusita kumsaidia. Maisha yangu yalikuwa
yamezungukwa ndugu wengi waliokuwa wakinitegemea katika mahitaji
mbalimbali ijapokuwa nilikuwa sina uwezo mkubwa sana kifedha. Lakini
nilijitahidi kwa kila hali kuhakikisha nawasaidia.
Baada ya miaka mitatu siku moja nikiwa
natoka kazini nilipata ajali nikiwa naendesha gari aina ya Corola, na
kunisababishia kuvunjika miguu, nilikuwa katika wakati mgumu sana kwani
nilikuwa sina uwezo wa kufanya kazi tena.
Na sasa nilikuwa nahitaji msaada kwa
ndugu zangu, lakini chakushangaza wale ndugu niliokuwa nawasaidia hata
sikumoja hakuna aliyekuja kunisaidia kwa chochote, walikuja kunisalimia
maramoja tu na baada ya hapo sikumuona tena ndugu yeyote. Siku moja
alikuja shemeji yangu na Mama mkwe kwa nia ya kumshauri mke wangu
aniache kwani sina uwezo wa kumsaidia. Niliumia sana moyoni "Inamaana
leo hii mimi Beni, naonekana sifai baada ya kupata ajali, na mbona
nilikuwa nikiwasaidia sana, hivi ni kweli wananichukia kiasi hiki. Mungu
nisaidie nipone, ama kweli binadamu hawatabiriki."
Mke wangu, alikuwa na msimamo na hivyo
hakuniacha aliendelea kuwa na mimi hivyohivyo. Ndugu zake walimtenga
kabisa, kwasababu yangu.Maisha yalliendelea baada ya mwaka mmoja
kupita, hatimaye nilipona kabisa nakurudi katika hali yangu ya kawaida.
Nilirudi katika kazi yangu ya awali bila matatizo. Kwani nilipokelewa
vizuri na sasa nilipandishwa cheo. Maisha yangu yalirudi katika ramani
nzuri, wale ndugu walionikimbia wakati naumwa, baada ya kusikia kuwa
nimerudi kazini. haikuchukua muda walianza kuja kunitembelea tena
wakijidai wamekuja kunijulia hali.Lakini kwasababu tayari nilikuwa
nimejifunza mambo mengi hivyo nilijua namna gani naweza kuishi nao.
Safari hii nilikuwa makini zaidi. Sikutaka kulipiza kisasi naishi nao
vizuri.
AMA KWELI BINADAMU HAWATABIRIKI, ANAWEZA KUKUPENDA UKIWA NACHO UKIWA HAUNA KITU ANAKUKIMBIA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni