SHAMRA shamra zilizidi kurindima kwa fujo katika ukumbi wa Sabasaba
wilayani Temeke, hakika maharusi walikuwa wamependeza na utakuwa mchoyo
wa kuzaliwa usingewapongeza waliotumia ubunifu wa hali ya juu kuupamba
ukumbi ule nao ukapambika.
Kila mmoja alitabasamu bila kujalisha linatoka moyoni ama ni la kuzugia!!
Wanawake walipiga vigelegele na wanaume walipiga mbinja kila muda ambapo msema chochote aliamuru!!
Naam!! Ilikuwa sherehe ya aina yake ya kuwaunganisha Maria na Christian kuwa mwili mmoja!!!
Chris alikuwa mwenye furaha sana alipopewa nafasai ya kusema chochote,
alizishukuru pande mbili akianza na ule upande wa ukweni akawashukuru
kwa zawadi ya mke mwema…..kisha akageukia upande wa pili na kuwashukuru
wazazi wake waliomkuza na kumpa elimu dunia pamoja na ile ya darasani!!!
Hatimaye msema chochote akamkabidhi kipaza sauti Maria!!
Ukumbi mzima ulitambua kuwa Maria hakuwa akitabasamu kutoka moyoni lakini bado hakuna aliyejua kwanini alikuwa katika hali ile.
Maria akashika kipaza sauti mbele ya umati na kuanza kuzungumza.
“Imekuwa safari ndefu sana hadi kuifikia siku hii ya leo…nikimtoa
mwenyezi Mungu katika safari hii ninaye mtu mwingine muhimu katika dunia
hii wa kumshukuru!! Ni mtu mmoja tu nasisitiza pasipokuwa na unafiki
wowote!!
Namshukuru mama yangu…mama yangu wa Kambo” akasita kidogo ukumbi nao ukawa kimya!! Kimya kikuu…Maria akaendelea.
“Asante sana mama wa kambo kwa MATUSI YOTE uliyonitukana maana
ulinifanya niyazoee, awali nilikuwa nakasirika sana ukunitukana,
ukimtukana marehemu mama yangu, ukinitukania baba yangu. Naam
ukaniimarisha zaidi hata nilipokuwa nafanya kazi za ndani sikuhangaishwa
na matusi kutoka kwa watoto wa bosi wangu!! Niliyapuuzia tu!!!
Asante kwa KUNILAZA NJE asante sana kwa jambo lile, nikalizoea giza, mbu
wakaizoea damu yangu!! Ukaniimarisha na hata nilipokosa pa kulala
nikiwa mtaani stendi ilikuwa sehemu sahihi kwangu na nililala bila hofu.
Mama wa kambo siwezi kusahau kukushukuru kwa kunilisha chakula ambacho
watoto wako walilalamika kuwa ni kibaya ama kimeharibika. Ulikuwa sahihi
mama maana hata kule majalalani sikuhangaika tena kila kinachoitwa
chakula mimi nilikula. Unadhani ungenidekeza ningeweza vipi?
Siku
uliyoamua rasmi kunifukuza ukinizushia kuwa nakujazia choo na
kukumalizia godoro bila sababu za msingi ni hivyo hivyo niliwahi
kufukuzwa na mabwana wengi walaghai. Lakini sauti zao na yako zilifanana
hivyo sikuogopa chochote kitu!! Nikabaki kuwa imara huku nikihesabu
kuwa haya ni mapito tu!!
Kulala bila kula kwa siku mbili hadi tatu
katika nyumba yako lilikuwa jambo la kawaida sana hivyo niliweza
kumvumilia Chriss wangu alipokuwa hana pesa. Alinishangaa sana kwa
uvumilivu wangu lakini leo atambue kuwa bila wewe nisingeweza
kumvumilia.
Ulininyima elimu mama wa kambo!! Vyema sana ukanifanya
niishi kwa kutumia nguvu zangu tu na akili ya ziada lakini si vyeti!!
Sikuwa mtu wa kuchagua kazi, nilibeba kokoto, nikafanya ubaamedi,
nikafua nguo za watu, nikafagia barabara na kazi zote zile ambazo
zilihitaji watu kama mimi nisiyekuwa na elimu!! Asante mama wa kambo!!!
Sijaisahau ile siku uliyonimwagia maji ya moto na kuondoka na ngozi
yangu usoni, tazama ulinisaidia sana hakika, wanaume hawakunitamani!!
Ndio…nani wa kumtamani na kumthamini mwanamke asiyekuwa na mvuto.
Ulifanya la maana sana mama maana maumivu niliyoyapata kuondokewa na
wazazi wangu, maumivu niliyoyapata kwa mateso yako, ni heri hayo
yalitosha na ukaniepushia maumivu ya kudanganywa na wanaume wakware kisa
uzuri wangu kisha wanitelekeze pasi na msaada. Ni heri waliidharau na
kuichukia sura yangu hadi nilipokutana na Chriss. Hakujali sura
akayajali maumivu yangu na akaamua kunipooza!!!
Hata lile kovu
uliloniachia kwa kunichoma na mkaa wa moto pajani, yeye hakujali pia.
Unadhani ni wanaume wangapi wanaweza kuwa na ujasiri wa Chriss??
Nasema nawe ewe mama uliyevaa nguo nyeupe pee!! Umeketi katika kiti cha
tatu kutoka kushoto, mama usiyekuwa na haya uliyenitukana huku ukisema
kamwe kuwa sitaolewa!! Nimezisikia tetesi kuwa wale wanao wawili wa kike
uliowabatiza cheo cha umalikia walijazwa mimba na kuzaliwa nyumbani,
sijui kama ni kweli kuwa yule mwanao wa kiume alinibaka ukanitusi mimi
kuwa namfunza tabia mbaya nasikia na yeye ni teja na kila leo anakuibia
vitu nyumbani!!
Natoa shukrani kwako kwa mabaya yote uliyonitendea,
natoa shukrani kwako kwa moyo wako mgumu unaodhani kuwa niliyasahau yale
yote na leo hii umeketi upande wa ukoo wangu ukisubiri kunipa zawadi ya
kunipongeza kwa sababu nimeolewa.
U mnafiki ewe mama, u mkatili katika maana halisi ya kuitwa mkatili.
Nayasema haya ili niwe na amani, nayasema haya bila unafiki wala
tabasamu bandia la kuigiza!!! Nilijua itafika siku ya kusema nd’o maana
sikusema katika siku hizi zote.
Ewe mama wa kambo umenipa zawadi
nyingi sana tena za kudunu, siihitaji zawadi yako siku hii ya leo.
Sihitaji chochote kitu katika maisha yangu kutoka kwako!! Umenipa vingi
na vinatosha sana!!!
Asante sana mama wa kambo!! Mama mbaya
unayesababisha hata wale mama wa kambo wenye utu waonekane kuwa si
lolote na si chochote kitu!!!”
Maria alimaliza kuzungumza huku machozi yakiondoka na nuru yake asiweze kuona mbele tena.
Mama yule ambaye ukumbi mzima ulikuwa ukimtazama alibaki akiwa
ameinama. Watu walingoja sana anyanyuke waweze kuibaini walau sura yake.
Lakini hakunyanyuka, aliyeamua kumgusa bega mara kadhaa kwa kumsukuma
ndo aliihitimisha safari yake sakafuni. Mama yule hakuwa na fahamu
zake!!!
Zikafuata hekaheka za kumpepea lakini fahamu hazikurejea.
Maria naye alifanya harakati hizo huku akiipuzia shela aliyokuwa
ametinga. Hali ilikuwa tete na ukumbi wa sherehe ukageuka kuwa ukumbi wa
hekaheka!!
Wakati mama yule anakimbizwa hospitali, Maria alipata
fursa ya kukwapua bahasha ambayo awali ilikuwa mikononi mwa mama wa
kambo kabla hajaanguka!!
Akaifungua na kukutana na kipande cha karatasi.
“Sina zawadi yoyote ya kukupa Maria, japo ni wewe wa kunipa mimi zawadi
kubwa ya msamaha. Hakuna nikitegemeacho tena duniani zaidi ya msamaha
wako!! Siwezi kujieleza nikaeleweka kwa yote yaliyotokea miaka hiyo
lakini waweza kunielewa! Ninauhitaji msamaha wakokabla sijafa Maria.
Nililelewa na mama wa kambo nikanyanyaswa na kupewa kila aina ya mateso,
sidhani kama ilikuwa sahihi kulipizia kwako nakiri mbele yako kuwa
nilikosa na leo hii nitaomba msamaha mbele ya umati. Nisamehe Maria!!”
Alipomaliza kuusoma ujumbe ule alihitaji kumwona yule mama na kumweleza
kuwa amemsamehe tayari lakini akakutana na taarifa kuwa MAMA WA KAMBO
AMEFARIKI TAYARI!!!
Maria alijikuta katika mkanganyiko wa huzuni na amani!!
“ASANTE MAMA WA KAMBO!!” akajisemea.
UJUMBE: Usifanye jambo ambalo wewe hupendi kufanyiwa na kisha
ukalibariki kwa kuliita KISASI……kila baya unalofanya nawe litakutukia
katika namna ya kustaajabisha!!!
Mama wa kambo ni mama ……japo wengine wanawachafua!!!
MWISHO!!!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni